De Gea: Tunataka Kushinda Kombe la FA
David De Gea ametamka kuwa 2015-16 ulikuwa msimu mzuri kwake Manchester United lakini anataka kumaliza na taji
Mlinda mlango wa Manchester United David De Gea amesema amekuwa na
msimu mzuri katika taaluma yake ya soka kwa mtazamo wake, lakini anataka
kumaliza japo na taji moja katika mechi ya fainali Kombe la FA
Jumamosi.De Gea alikaribia kuondoka Old Trafford siku ya mwisho kabla ya kufungwa dirisha la usajili wa majira ya joto kutimkia Real Madrid lakini mkanganyiko wa nyaraka ukamkwamisha.
Lakini hakutaka mambo ya usajili yamvuruge, aliendelea kufanya kazi yake nzuri United, na amechangia kwa kiwango kikibwa kuiwezesha Manchester United kutinga fainali ya Kombe la FA na kumaliza nafasi ya tano Ligi Kuu.
Ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa United kwa mara ya tatu, na kuwa kipa wa pili Ligi Kuu Uingereza huku wa kwanza akiwa Czech wa Arsenal.
“Umekuwa msimu bora katika maisha yangu ya soka,” alisema De Gea. “Niko vizuri kimwili na kiakili.
“Kama tukitwaa Kombe la FA utakuwa msimu mzuri. Sote tunataka kutwaa taji hilo muhimu kwa ajili ya mashabiki wetu na kwa ajili yetu binafsi kama wachezaji. Tutapambana hadi mwisho na kufanya kila kinachowezekana kutwaa taji hilo.”
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania amesema kutwaa Kombe la FA kutaisaidia United kumaliza msimu mgumu waliokuwa nao kwa furaha na huenda ukajenga bahati kwa ajili ya msimu ujao.
“Tumekuwa na msimu mgumu na tumedhamiria kuibuka na kombe,” aliongeza.
“Na kushinda kutatupa kila sababu ya kujivuna na kutuongezea hamasa na tumaini la kufanya makuu zaidi.”

Maoni
Chapisha Maoni