Kumbukumbu ya miaka 100 ya mapambano ya Verdun
Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa Jumapili (29.05.2016) wameshiriki
kumbukumbu ya miaka 100 ya Mapambano ya Verdun kwa kuweka shada la maua
katika makaburi ya wanajeshi 300,000 wa nchi hizo waliouwawa.
Mapambano ya Verdun ni mojawapo ya mapambano yaliochukuwa muda mrefu
katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia ambapo yalidumu kwa siku 300
kuanzia Februari hadi Disemba mwaka 1916. Mapambano hayo kaskazini
mashariki ya Ufaransa licha ya kuwa makali kabisa na kugharimu maisha ya
wanajeshi 163,000 wa Ufaransa na wanajeshi 143,000 wa Ujerumani
yalishindwa kutowa mshindi.Miongoni mwa matukio ya mwanzo ya kumbukumbu hiyo viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa waliweka shada la mauwa katika makaburi ya wanajeshi wa Ujerumani huko Consenvoye kaskazini mwa mji wa Verdun ambapo miili ya wanajeshi wa Ujerumani ilizikwa.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani walihudhuria hafla katika Ukumbi wa jiji huko Verdun ambapo katika hotuba yake Merkel amesema Verdun inasimamia sio tu "unyama usioelezeka na upuuzi wa vita " bali pia "kutowa mafunzo na usuluhishi wa Ujerumani na Ufaransa."
Mapambano ya Verdun ni funzo
Amesema "ni wale tu wanaojuwa kipindi cha kale wanaweza kujifunza kutokana na hayo na kutumia jambo hili kujenga mustakbali mwema" na kuongeza kwamba dhana ya urafiki aliyoipata katika mji huo akiwa kama kansela wa Ujerumani "haifai kabisa kuchukuliwa kijuu juu".
Yeye na Hollande pia walimkabidhi Meya wa Verdun Tuzo ya mwaka huu ya Adenauer - de Gaulle ambayo hutunukiwa wale wanaochangia kujenga uhusiano mzuri kati ya Ujerumani na Ufaransa.
Hollande amesema Verdun sio kitu kilichoganda na mahala pa kutukuzwa kwa wafu bali daima imekuwa ikiangalia mbele kwa matumaini kutimiliza lengo lake la amani.
Watoto wa Ufaransa na Ujerumani takriban 3,400 wamepangiwa kuwasilisha mhadhara katika hafla ya kimataifa huko Douaumont ambapo miili ya wanajeshi 130,000 iliobakia kutoka pande zote mbili imezikwa.
Umuhimu wa Douaumont
Kumbukumbu ya mapambano hayo imekuja kuashiria uhusiano wa karibu uliopo kati ya Ufaransa na Ujerumani. Ni mwaka 1984 nchi hizo jirani ndipo zilipokubali kufanya hafla ya pamoja ya kumbukumbu ya mapambano ya Verdun ikiwa ni hatua nyengine mbele ya kukomesha uhasama na kutokuaminiana kati ya mataifa hayo mawili baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu Viwili vya Dunia.
Mwaka huo pia ulishuhudia bunge la Ulaya likipitisha mkataba wa kuanzisha Umoja wa Ulaya na makubaliano kati ya Ufaransa na Ujerumani kuondowa ukaguzi wa mipaka hatua kwa hatua.
Changamoto kwa Umoja wa Ulaya
Akizungumza katika mkesha wa kumbukumbu hii Kansela Merkel amesema ukweli kwamba amealikwa kuhudhuria kumbukumbu hiyo mwaka huu ni ishara jinsi uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ulivyo mzuri hivi sasa.
Ujerumani na Ufaransa zinaonekana kuwa engini kuu ya Umoja wa Ulaya unaoundwa na mataifa wanachama 28 ambao hivi sasa unakabiliwa na changamoto kubwa kama vile wimbi la wahamiaji na wakimbizi wanaokimbilia Ulaya na misukosuko ya kifedha inayozikumba baadhi ya nchi wanachama.
Uwezekano wa kujitowa kwa Uingereza kutoka umoja huo umezidi kuongezea hisia iliozagaa kwamba umoja wa kundi hilo uko hatarini.
Maoni
Chapisha Maoni