Tabia 8 za wazazi ambazo huenda zikawafanya watoto wasifanikiwe vizuri kimaisha
Kuzaa sio kazi,
kazi kulea mwana, waswahili walisema. Kama mzazi ni jukumu lako
kuhakikisha mwanao anakua katika mazingira mazuri na elekezi kwakwe
kumfanya awe ni mwenye hekima kuanzia mdogo mpaka katika utu uzima wake.
Kulea ni kazi, tena asikuambie mtu ni kazi kubwa sana kulikoni hata
ya kubeba zege. Kumkuza mtoto mdogo awe vile unavyotaka kupitia
muonekano wako au mtazamo wako ni kitu kikubwa sana na kama unajiona uko
hivyo ulivyo sasa kwa sababu ya wazazi wako washukuru. Maana si kazi
ndogo waliofanya.
Kuna vitu kadha wa kadha ambavyo vinaweza kuchangia katika ukuaji au
malezi kwa namna moja au nyingine. Mfano mazingira unayoishi, hali ya
kijamii na uchumi wa familia, na vile vile elimu ya wazazi wanaomlea
mtoto.
Ni vigumu kujua njia ipi ya malezi itakuwa sahihi, ila kuna tabia za
wazazi za aina Fulani ambazo wanasayansi wamegundua inaweza kuathiri
malezi ya mtoto kwa njia chanya ama hasi.
Zifuatazo ni tabia ambazo wazazi wengi wanazo ambazo hupelekea watoto wao wasifanikiwe maishani.
- Wazazi wasio wahamasisha watoto wao kujitegemea/ kuwa huru.
Wazazi wanashauriwa kuwahimiza watoto wao kuwa wenye kujitegemea
kimawazo na kujiamini, hii inasaidia sana hata anapokutana na vishawishi
katika rika lake, ajue lipi baya lipi zuri. Unapomwamulia kila kitu
haumjengi, unamjenga mtoto endapo utamfanya ajiamini na kujitegemea.
Kumbuka kwamba hautaishi nae milele, jifunze sasa kumwacha huru katika
maamuzi madogo atajiamini kutatua matatizo yake binafsi
2. Wazazi wanaokaripia watoto wao mara kwa mara.
Unapokuwa unatumia maneno makali makali kila mara mtoto awapo
amekosea kuna madhara ya muda mrefu. Kumkaripia mtoto, kumtukana,
kumsema kwa kejeli humfanya mtoto awe kwanza muoga wa kila kitu au
tuseme si mthubutu, hii peke yake imtarudisha nyuma katika makuzi yake
na vile vile kama mzazi, jaribu kutafuta njia mbadala ya kumfunza mtoto
maana kuna usemi unasema ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’, mtaanza
kufokeana ndani ya nyumba akifikia umri wa balehe na kumbe lilikua kosa
lako.
3. Tabia ya mzazi utaka kujua kila kitu kinachoendelea katika maisha ya mtoto.
Sawa ni kitu kizuri kwa upande mwingine, unakua
haukosei sehemu yoyote ya maisha ya mwanao lakini kuendesha kila kitu
chake kutampelekea mtoto awe na wasiwasi na huzuni kupindukia. Hawezi
kufanya uamuzi wowote ule katika maisha yake bila wewe kuwepo, unakuta
mama au baba walitaka kuwa madaktari ikashindikana, wanalazimisha sasa
ndoto zao zitimizwe na mtoto na yeye kwa uoga wa kuwasaliti
anang’ang’ania fani ambayo wala haiwezi maskini, ni lazima tu atafeli,
tena sio shule tu, anafeli hadi maisha. Maana muda wake mwingi anautumia
kufanya kitu ambacho hakina manufaa kwake kwasababu tu mzazi alisema.
- Kumuacha mtoto aamue mwenyewe muda wa kulala.
Wenzetu wazungu ndio wanalifatilia sana, lakini ni
kitu kimoja muhimu sana, ukuaji wa ubongo wa mtoto mdogo wanasayansi
wanasema unahitaji fomula, mtoto hawezi kuamua mwenyewe alale saa mbili
usiku kila siku, leo atalala saa moja kama alichoka sana, kesho atalala
saa 3 kama kwenye TV kulikua na kipindi anachopenda kukiangalia, na siku
nyingine atalala hata saa sita ukiamua umuache mwenyewe aamue. Mpangie
muda wa kulala usiopungua masaa 9-10 usiku hili litamsaidia hata akiamka
kuwa mwenye nguvu za kujifunza vitu vipya na ubongo wake utakua kwa
nafasi.
- Kumuacha mtoto angaalie TV akiwa mdogo sana.
Watoto wanaongalia TV wakiwa na umri chini ya miaka 3 huathirika sana
katika jinsi wanavyoongea, au kushiriki na watoto wengine. Tunaweza ona
kwa sasa ni njia rahisi ya kulea maana unamwacha anakodolea TV hapo we
unaendelea na kazi nyingine, la hasha, hilo liache mapema sana, TV
inaonyesha mengi, vurugu, lugha za matusi, picha zisizofaa kwa watoto
yote haya yanaingia kwenye kichwa chake na kuanza kujenga tabia ambazo
atakua nazo, na najua tu hatutazipenda. Jaribu kusomea vitabu, una kazi
zimekubana amezoea vitabu atafunua vitabu vyake ataangalia picha
akishindwa atacheza na toys zake. Ana muda mwingi sana wa kuja kuangalia
TV badae.
- Wazazi wanaotumia mabavu:
Mzazi anayetumia mabavu ni yule anayetoa amri moja,
na usipoifata utaona cha mtema kuni, mfano anaposema ‘ufaulu mtihani la
sivyo ukifeli usirudi nyumbani’ . Kwa wakati mwingine mzazi mwenye
mamlaka na mwenye kutaka aeleweke kwanini amesema hivyo ujumbe wake
utatoka kwa namna tofauti, mfano ‘inakulazimu ufaulu mtihani, maana watu
wote walifanya vizuri mashuleni wana maisha mazuri baada ya shule’.
Hawa ni wazazi wawili tofauti. Ulezi wa kutumia mabavu haujengi hata
kidogo, sasa kwa mfano mtoto kafeli ndio, alafu harudi nyumbani si
ataishia kuwa mtoto wa mtaani, au kibaya zaidi kuwa kibaka.
- Kutokuwa karibu na mtoto au kutokumpa mapenzi mtoto.
Hakuna kinachoweza kuwa badala ya mapenzi au uwepo wako kwa mtoto
wako, tena hii ni kiafya na makuzi ya kawaida. Tengeneza ukaribu na
mwanao, mpe mapenzi aone kama kweli duniani wazazi ndio wanatufunza
mapenzi. Watu wengi wanamatatizo ya kutokuamini watu, au kutokufungua
hisia zao na kuruhusu kupendwa kwa vile tu wazazi wake hawakumfanya aone
ni kawaida kuachia moyo huru ukapenda au kupendwa.
Na vile vile kumpongeza mtoto wako anapofanya vizuri, au
kumwambia/kumuonyesha mwanao unampenda ni muhimu katika makuzi ya mtoto
mdogo, kwanza halikupunguzi kitu, bali linakuongezea ukaribu na mwanao.
- Wazazi wanaotumia fimbo kumuelimisha au kumfunza mtoto
Fimbo au vibao havijawahi kuwa njia mathubuti ya kumfunzia mtoto, kwa
upande mwingine kwanza unakuwa umezidiwa busara na mtoto mdogo mpaka
unapandwa na hasira za kuchapa. Kama wewe uko hivyo, unategemea yeye
atakuja kuwa vipi? Si ndo wa kushikana mashati na wenzie mtaani?.
Uchunguzi unasema, kumchapa mtoto hakumfunzi, bali kunamfanya awe sugu
na badae watoto hawa huishia kuwa mazezeta na wenye kushindwa
kujitambua.
Wewe kama mzazi una nafasi kubwa ya kuamua namna mtoto wako
atakavyokuja kuwa baadae. Kumbuka “Samaki mkunje angali mbichi,” “Mtoto
umleavyo ndivyo akuavyo.
Maoni
Chapisha Maoni