KEPTENI wa England Wayne Rooney amemtetea Meneja wake Roy Hodgson na kusisitiza Wachezaji wote wanaheshimu uamuzi wake wa kubadili Wachezaji 6 walipotoka Sare 0-0 na Slovakia Juzi Jumatatu katika Mechi ya Kundi B la EURO 2016 huko France.
Licha ya kuwepo ripoti kuwa Rooney, ambae aliingizwa Kipindi cha Pili kwenye Mechi hiyo na Slovakia, alishangazwa na kutemwa kwake, mwenyewe Rooney amesisitiza Kambi ya England iko burdani.
Rooney ameeleza: “Naheshimu uamuzi wa Roy. Kama Mchezaji unataka kucheza lakini kwenye Raundi ijayo dhidi ya Iceland nitakuwa freshi zaidi!”
Mbali ya kupumzishwa Rooney kwenye Mechi hiyo na Slovakia, Hodgson pia aliwatema Kyle Walker, Danny Rose, Dele Alli, Raheem Sterling na Harry Kane na Droo hiyo ikatoa mwanya kwa Wales kutwaa ushindi wa Kundi B.
Hilo likafanya Wales waikwae Northern Ireland kwenye Raundi ya Mtoano ya Timu 16 ya EURO 2016 na England wataivaa Iceland kwenye Raundi hiyo hiyo Jumatatu ijayo huku Washindi wakitinga Robo Fainali.
Rooney ameongeza: “Nadhani ni uamuzi ambao Roy alifanya ili kupumzisha Wachezaji na kwa kuamini Kikosi chake. Nakubaliana nao. Wachezaji waliopangwa hawakuwa wazuri kushinda Mechi lakini vile vile wapinzani walijihami vizuri.”
Ikiwa Rooney atacheza Jumatatu ijayo dhidi ya Iceland, itakuwa Gemu yake ya 115 kwa England akifungana na David Beckham na kuwa wa Pili katika Listi ya Kihistoria ya Wachezaji waliochezea Mechi nyingi England ambayo inaongozwa na Kipa Peter Shilton aliecheza Mechi 125.
Rooney ameeleza: “Nimesema mara nyingi kwamba ni heshima kubwa kuwa Kepteni wa Nchi yangu na ni kitu daima najaribu kukifanya kwa uwezo wangu wote na kwa fahari kubwa!”

Maoni
Chapisha Maoni